Tuesday, October 5, 2021

 


KOCHA Mdenamrk, Kim Poulsen amewaongeza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wachezaji wawili, beki Kibwana Shomari wa Yanga na mshambuliaji Kibu Dennis wa Simba SC.
Wawili hao wameongezwa kuelekea mchezo wake wa tatu wa Kundi J kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Benin keshokutwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Na hiyo ni baada ya kiungo Jonas Mkude kuomba udhuru wa matatizo ya kifamilia – lakini wachezaji wengine watatu mabeki Bakari Mwamnyeto wa Yanga na Shomari Kapombe na Erasto Nyoni wa Simba waliripoti wakiwa majeruhi, hivyo wameruhusiwa kurejea kwenye klabu zao kuendelea na matibabu.


Nahodha Mbwana Samatta anayechezea Royal Antwerp ya Ubelgiji aliwasili jana usiku, wakati Simon Msuva wa Wydad Athletic ya Morocco amewasili mapema leo.
Baada ya kuvuna pointi nne katika mechi mbili za awali kutokana na sare ya ugenini 1-1 na DRC Lubumbashi na ushindi wa nyumbani wa 3-1 dhidi ya Madagascar, Taifa Stars inaongoza Kundi J ikifuatiwa na Benin pointi nne pia, DRC pointi mbili na Madagascar ambayo haina pointi. 

0 comments:

Post a Comment