Meneja wa Habari wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally ameendelea kusisitiza suala la kutokua na wasiwasi wa kutetea ubingwa msimu huu, licha ya kuachwa kwa alama 10 na YoungA fricans.


Simba SC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 25, ikitanguliwa na Young Africans ikiwa kileleni kwa alama 35 baada ya kushuka Dimbani mara 13.


Ahmed Ally amesema bado wana matumaini makubwa ya kutetea taji la Ligi Kuu kwa mara ya tano msimu huu, na wanajua ni muda gani wa kumshusha Young Africans kileleni.


“Gape la Point 10 halitutishi kabisa, ilimradi aliyekua juu ni Yanga, sisi tunajua ni wakati gani tutamshusha tu.” ameandika Ahmed Ally kwenye ukurasa wake wa Instagram.


Simba SC kesho itacheza mchezo wake wa kiporo dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba, baada ya mchezo huo kuahirishwa Desemba 12 mwaka 2021, kutokana na wachezaji wengi wa Simba SC kukutwa na maambukizo ya ugonjwa wa mafua, kukohoa, kichwa na homa kali.


Wakati huo huo kikosi cha Simba SC kimefika salama mjini Bukoba kikitokea Jijini Dar es salaam kwa usafiri wa Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania ‘Air Tanzania.