Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC kupitia Mtendaji Mkuu ‘CEO’ Barbara Gonzalez, amesema mbali na ndani ya uwanja, klabu hiyo inakutana na vita kubwa nje na kupambana kuishinda.
Barbara ametoa kauli hiyo baada ya kukiri ukweli wa kufunguliwa mashtaka na Afisa wa Bodi ya Ligi ‘TPLB’ Jacqueline Kimwemu kwa madai ya kumtolea lugha chafu.

Amesema ameshtusha na taarifa hizo baada ya kupokea barua siku ya Alhamisi (Januari 20) na kuhojiwa na jeshi la Polisi kwa madai hayo, jambo ambalo anaamini ni vita katika Soka.

“Nilishtushwa sana kwa sababu tukio hilo limetoka Desemba mwaka jana ‘2021’ na sasa ni Januari na tayari nimeshatumikia adhabu ya TFF kwa kulipa kiasi cha fedha, lakini nimeshangazwa na tukio hili.”

“Siwezi kujua tukio hilo kuna nini nyuma yake, lakini siko peke yangu na nitahakikisha natoa ushirikiano mzuri Polisi kurahisisha uchunguzi wao.”

“Hii ni vita kubwa zaidi na nzito tutaendelea kupambana, kwa sababu vita hivi haviishii uwanjani hata nje ya uwanja pia, tunapambana kuhakikisha tunashinda na kusonga mbele katika malengo yetu,” amesema Barbara.

Amesema ana imani suala hilo lilikuwa chini ya mamlaka ya sheria, hukua kiahidi kuwa sehemu ya safari mkoani Kagera katika mchezo wao wa kesho Jumatano (Januari 26) hii dhidi ya Kagera Sugar.