Saturday, January 8, 2022

 


MABINGWA wa Tanzania, Simba SC wamefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi licha ya sare ya 0-0 na wenyeji, Mlandege FC jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Simba inamaliza kileleni mwa Kundi C kwa pointi zake nne, mbili zaidi ya Mlandege hivyo inatinga Nusu Fainali na itakutana na mshindi wa pili wa Kundi A Jumatatu.
Mechi iliyotangulia, mabingwa watetezi, Yanga SC wametinga Nusu Fainali pia licha ya sare ya 2-2 na wenyeji wengine, KMKM hapo hapo Uwanja wa Amaan.
Yanga wamekwenda Nusu Fainali kwa kuwazidi KMKM wastani wa mabao tu baada ya timu zote kuvuna pointi nne.
Tayari Kundi A zote Azam na Namungo zimefuzu Nusu Fainali baada ya kila timu kukusanya pointi nne.
Namungo imekamilisha mechi zake, wakati Azam FC wanacheza mechi ya mwisho dhidi ya Yosso Boys kesho.
Mshindi wa kwanza wa Kundi A atamenyana na mshindi wa kwanza wa Kundi B, ambaye ni Yanga wakati mshindi wa pili wa Kundi B atamenyana na mshindi wa kwanza wa Kundi C, ambaye ni Simba.

0 comments:

Post a Comment