Sunday, January 2, 2022

 



MABINGWA watetezi, Simba SC wameuanza vyema mwaka 2022 baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Baada ya dakika 45 kumalizika bila mabao huku kiungo Mzambia, Rally Bwalya akikosa penalti iliyopanguliwa na kipa Mzanzibari, Ahmed Ally Suleiman’Salula’ dakika ya 14 baada ya winga Msenegal, Pape Ousmane Sakho kuchezewa rafu na kiungo Frank Raymond Domayo, milango ilifunguka kipindi cha pili.
Ni kiungo wa kimataifa wa Mali, Sadio Kanoute aliyefunga bao la kwanza la Simba dakika ya 68, kabla y Sakho kufunga la pili dakika ya 72 na Azam FC ikapata bao lake pekee kupitia kwa mshambuliaji Rodgers Kola dakika ya 80.
Simba SC inafikisha pointi 24 katika mchezo wa 10, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi tano na watani wao, Yanga ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi, wakati Azam FC inabaki na pointi zake 15 za mechi 11 sasa katika nafasi ya saba.

0 comments:

Post a Comment