Saturday, January 8, 2022

 







MABINGWA watetezi, Yanga SC wamefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi licha ya sare ya 2-2 na wenyeji, KMKM jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mabao ya Yanga ambayo mara zote ilitangulia yalifungwa na mshambuliaji Mkongo, Heritier Ma Olongi Makambo dakika ya 45 na kiungo Mzanzibari, Feisal Salum Abdallah dakika ya 81, wakati ya KMKM yamefungwa na Adam Ibrahim Abdallah dakika ya 54 na Kheri Makame Jecha dakika ya 90 na ushei.
Kwa matokeo hayo, timu zote zinamaliza mechi za Kundi B na pointi nne kila moja baada ya mechi mbili, lakini Yanga wanakwenda Nusu Fainali kwa kuwazidi wastani wa mabao KMKM wameruhusu mabao moja zaidi ya mabingwa hao watetezi.
Tayari Kundi A zote Azam na Namungo zimefuzu Nusu Fainali, wakati Simba SC inahitaji sare tu katika mechi yake ya mwisho ya Kundi C dhidi ya Mlandege usiku wa leo ili kwenda Nusu Fainali.
Mshindi wa kwanza wa Kundi A atamenyana na mshindi wa kwanza wa Kundi B, ambaye ni Yanga wakati mshindi wa pili wa Kundi B atamenyana na mshindi wa kwanza wa Kundi C.

0 comments:

Post a Comment