KLABU Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka sare ya bila kufungana dhidi ya
Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL)
uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Huo ni mchezo wa kwanza wa
kihistoria kwa timu hiyo kuweza kucheza katika uwanja wake wa nyumbani
dhidi ya Simba, ambao ulitawaliwa kwa ubabe kwa pande zote mbili huku
Refari akionesha kadi za njano kama jungu.
Ulikuwa ni mchezo wa kugawana
vipindi, ambapo Azam FC ilionekana kutawala kipindi cha pili huku
wapinzani wao wakitawala kipindi cha kwanza na pande zote zikikosa
mabao.
Winga wa Azam FC, Enock Atta,
alipiga shuti la umbali dakika ya 18 lilidakwa na kipa wa timu hiyo,
Aishi Manula, ambaye alikuwa akirejea kwa mara ya kwanza Azam Complex
tokea asajiliwe na Simba msimu huu akitokea kwa mabongwa hao,
Wachezaji wengine waliokuwa
wakirejea ndani ya viunga hivyo, ni gwiji wa Azam FC John Bocco
‘Adebayor’ na Erasto Nyoni, waliosajiliwa pia wakitokea kwa mabingwa hao
wa Afrika Mashariki na Kati.
Dakika ya 33 Atta alimsetia pasi
nzuri Yahaya Mohammed, alliyeingia na mpira huo ndani ya eneo la 18
lakini shuti alilopiga lilitoka sentimita chache ya lango na kuufanya
mchezo huo kumaliza kipindi cha kwanza kwa suluhu hiyo.
Mabadiliko yaliyofanywa na benchi
la ufundi la Azam FC ya kumuingiza kiungo Frank Domayo na kupumzishwa
Atta yaliiongezea ubora timu hiyo kwenye eneo la kiungo hali
iliyowafanya kutawala mchezo huo.
Dakika ya 63 Azam FC ilipata pigo
baada ya beki wake wa kulia, Daniel Amoah, kuumia na nafasi yake
kuchukuliwa na Ramadhan Singano ‘Messi’, mabadiliko hayo yalimlazimu
nahodha Himid Mao, kuhamia beki wa kulia na eneo la kiungo kubakia
Stephan Kingue, Domayo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Dakika 10 za mwisho za mchezo huo,
Yahaya Mohammed na Sure Boy, almanusura waipatie mabao Azam FC, lakini
shuti alilopiga kiungo huyo lilitoka sm chache ya lango na kichwa
alichopiga Yahaya kiliweza kudakwa na kipa.
Sare hiyo inaifanya Azam FC kupata
pointi moja na kufikisha jumla ya pointi nne ikisogea hadi nafasi ya
tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo sawa na Tanzania Prisons na Simba
zilizokuwa juu yake kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi
cha Azam FC kitapumzika kesho Jumapili kabla ya kurejea mazoezini
Jumatatu jioni tayari kabisa kujiandaa na mtanange ujao dhidi ya Kagera
Sugar, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Septemba 15 saa 1.00 usiku.
0 comments:
Post a Comment