Friday, September 8, 2017


Jumamosi ya September 9, 2017 kutakuwa na moja ya mechi nzuri na ya aina yake ya ligi kuu Tanzania bara ambapo Simba watakuwa wakicheza dhidi ya Azam kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Azam Complex pale Chamazi.
Mechi hii inapambwa na vitu vingi, ukiachana na upinzani uliopo kati ya timu hizi mbili, kitu kingine ni wachezaji wa Simba waliosajiliwa toka Azam watakuwa wakirejea kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wao wa zamamani lakni safari hii wakipambana kuiangamiza Azam.
Aishi Manula amelelewa na kukulia Azam FC, uwezo wake uwanjani na jina lake vyote vimejengwa akiwa Azam kumbuka huyu ni mshindi wa tuzo ya golikipa bora wa ligi msimu uliopita lakini golipipa namba moja wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Erasto Nyoni ni mchezaji aliyedumu Azam tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2017 alipohamia Simba ni mchezaji pia wa timu ya taifa. Shomari Kapombe ataukosa mchezo huo kutokana na majeraha yanayomkabili.
Tuachane na hao samaki ‘wadogowadogo’ sasa tumwangalie ‘papa’ huyu si mwingine ni John Raphael Bocco au ‘Adebayor’ unaweza kumwita Mr. Azam pia na ukaeleweka. Kama akipata nafasi ya kucheza atakuwa akicheza kwa mara ya pili akiwa analishambulia goli la Azam lakini itakuwa ni mara ya kwanza kulishambulia goli la Azam akiwa mchezaji wa ligi kuu.
Bocco ana historia kubwa yenye heshima ya juu ndani ya kikosi cha Azam, ukitaja mafanikio ya Bocco lazima uitaje Azam na Azam imepata mafanikio yake mgongoni kwa Bocco mchezaji mwenye kila sifa ya kuigwa na vijana wanaochipukia.
Baada ya kuwaumiza Azam wakamsajili Bocco
Ilikuwa mwaka 2007 Jonh Bocco alipocheza dhidi ya kikosi cha Azam FC wakati huo alikuwa bado ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Tegeta huku akicheza timu ya Cosmopolitan. Ilikuwa ni mechi ya ligi ya Wilaya ya Ilala iliyochezwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari Benjamin Mkapa.
Mguu wa Bocco ukaiua Azam kwa mabao mawili safi yaliyowamaliza Azam. Magoli hayo yakampa ulaji Bocco baada ya Azam kuamua kumsajili na kumjumuisha kwenye kikosi chao kilichoshiriki ligi ya mkoa kisha baadae ligi ya taifa.
Azam lipangwa kituo cha Dodoma kundi ambalo lilikuwa na timu za Majimaji ya  Songea, Kijiweni ya Uyole Mbeya, Mbagala Market pamoja na wenyewe Azam FC.
Magoli yake yanaipandisha Azam ligi kuu Tanzania bara.
Mechi ambayo ilikuwa ya kuamua ni timu gani itafuzu kucheza ligi kuu Tanzania bara ilikuwa ni Azam vs Majimaji ambapo mwanaume huyu alitupia bao mbili kwa mguu wake na kuipandisha Azam kucheza ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Bocco anakuwa Mr. Azam
Kwenye mafanikio yote ya Azam huwezi kuliepuka jina la Bocco, mchezaji ambaye alikuwepo tangu timu haijapanda daraja kucheza ligi kuu hadi kuwa timu ya kuwania mataji ya Afrika.   Mwaka 2012 Azam walishinda kombe lao kubwa la kwanza, walipotwaa taji la Mapinduzi na kuanzia hapo alikuwa adui wa Simba na Yanga.
Kwenye hatua ya makundi Bocco alitupia bao moja wakati Azam ikishinda 3-0 dhidi ya Yanga, wakafuatia Simba katika hatua ya nusu fainali wakachezea 2-0 Bocco akifunga bao la kwanza.
Mechi ya fainali Bocco akaweka bao la kwanza na kuisaidia Azam kushinda taji la Mapinduzi kwa ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Pemba.
Hakuna ubingwa ambao Azam wameshinda bila Bocco kufunga goli siku ya mechi ya ubingwa ukiachana na ubingwa wa Mapinduzi Cup 2017. Kwa maana hiyo Bocco amefunga kwenye mechi zote zilizoamua ubingwa isipokuwa Mapinduzi 2017.
Alifunga fainali ya Mapinduzi Cup 2012, akafunga mechi ya Azam kutangaza ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara 2014 dhidi ya Mbeya City, akafunga kwenye fainali ya Kagame Cup 2015.
Bocco hajawahi kuziacha salama Simba na Yanga
Ameshawaumiza sana Simba na Yanga, amewatoboa mabao 13 kila mmoja katika mechi ambazo amekutana na vilabu hivyo akiwa anacheza Azam FC.
Baada ya kudumu kwa miaka 10 Shujaa anaondoka
Hakuna hata mmoja miongoni mwetu aliyewahi kufikiri ipo siku John Bocco ataondoka Azam na kusajiliwa na timu ya Tanzania kisha badae kucheza dhidi ya Azam FC timu ambayo ukiitaja huachi kumtaja Booco.
Bocco alisani Simba baada ya mkataba wake kumalizika lakini pande mbili (Bocco na Azam) hawakufikia makubaliano ya mkataba mpya ndipo akaamua kuondoka kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.
Jumamosi hii atakuwa anarejea kwenye uwanja wake wa nyumbani wa zamani lakini safari hii atakuwa ni adui wa kuchungwa na mabeki pamoja na viungo wa Azam ili asiwafunge, lakini miezi kadhaa nyumba walikuwa wanamtengenezea mazingira ya kufunga.
Atakutana na swahiba wake kipenzi
Himid Mao ni miongoni mwa marafiki wakubwa wa John Bocco, kumbuka Bocco akiwa nahodha wa Azam msaidizi wake alikuwa ni Himid. Hawa jamaa pia walikuwa wanaishi chumba kimoja wakati timu inapokuwa kambini kwa hiyo unaweza ukaona ukaribu wao ni wa namna gani. Kwa namna moja au nyingine Bocco na Himid watakuwa wameumia kutengana ndani ya Azam baada ya kuwa pamoja kwa muda mrefu.

0 comments:

Post a Comment