Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura jana Jumatatu Septemba 18,
2017 ametembelea Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Mhe. Naibu Waziri Anastazia
Wambura ambaye aliongozana na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania
(BMT), Bw. Mohammed Kiganja alilakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Bw.
Kidao Wilfred.
Mhe. Naibu Waziri Anastazia
Wambura alifanya mazungumzo na Kidao kwa muda ambako alijifunza mambo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ripoti ya utendaji katika mwezi
mmoja tangu uongozi mpya wa TFF uingie madarakani.
Mhe. Naibu Waziri baada ya
kupata maelezo ya Utendaji kwa Uongozi mpya amepongeza Uongozi mpya kwa
kuanza vizuri na ameridhishwa na mipango ya Uongozi mpya katika program
za Vijana na Soka la Wanawake.
Pia amepongeza zoezi la
Ugawaji wa mipira 100 kwa mikoa yote ya Tanzania na kusema muhimu ni
kutumika ilivyokusudiwa. Anaamini mwanzo mzuri wa Rais Wallace Karia ni
dalili njema za kuleta maendeleo makubwa katika soka.
Mbali ya kuzungumza na Kaimu
Katibu Mkuu, Naibu Waziri Wambura alikuwa shuhuda wa mazoezi ya jioni ya
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti
Boys’ kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mara baada ya mazoezi hayo,
Naibu Waziri Anastazia alikaribishwa kuzungumza na vijana wa Serengeti
Boys, ambako awali kabisa alitaka vijana hao ambao wengi wao wana umri
wa chini ya miaka 15 kwa sasa kuwa ni wenye thamani.
“Mtakumbuka kamba kwee
Umitashumta mlikuwa wengi, ila mmebaki ninyi. Nataka mjue kuwa Serikali
iko hapa na tunafuatilia. Tunataka matunda kutoka kwenu,” amesema Naibu
Waziri, huku akiwapa salamu za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Dk. Harrison Mwakyembe.
Akaongeza: “Nawapongeza sana
kwa kuonesha mnaweza. Ila fanyeni mazoezi kwa juhudi, chezeni mpira kwa
uhodari, ila msisahau kuzingatia pia masoma. msifanye masihara hata
kidogo. Mkizingatia masomo na kucheza mpira, mtafanya makubwa zaidi.
“Naamini baada ya kambi hii
mtakuwa vizuri. Je, kwenye mashindano yajayo mtashika namba gani?”
alihoji Naibu Waziri Wambura kabla ya vijana kwa pamoja kujibu: “Namba
moja.”
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF), liliiteua Tanzania kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tayari
Tanzania imeanza kuandaa timu.
0 comments:
Post a Comment