Timu ya Taifa ya wasichana wenye
umri wa chini ya miaka 20 (Tanzanite), imewasili salama nchini ikitokea
Nigeria ambako ilicheza mechi ya awali dhidi ya wenyeji Nigeria katika
mchezo wa kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Ufaransa.
Timu hiyo iliwasili saa 9.00 usiku
wa kuamkia Jumanne Septemba 19, 2017 na kulakiwa na Kaimu Katibu Mkuu
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Kidao Wilfred; Bw.
Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano, Bw. Jonas Kiwia na Ofisa Habari wa TFF,
Bw. Alfred Lucas.
Mara baada ya kurejea, Kocha
Mkuu wa timu hiyo, Sebastian Nkoma, amesema walipoteza mchezo wa awali
kwa kufungwa mabao 3-0 kwa sababu Nigeria ni timu bora na Tanzanite kwa
sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
“Kwa kuwa tulionesha kiwango
bora, ni matumaini yangu kwamba tutafanya vema kwenye mchezo wa
marudiano hapa nyumbani na tutasonga mbele,” amesema Nkoma ambaye ndoto
zake ni kuipeleka Tanzanite Ufaransa mwakani.
Mchezo wa marudiano utafanyika Oktoba mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Wakati timu ikionekana ina ari
ya kufanya vema kwenye mchezo wa marudiano, Kaimu Katibu Mkuu, Bw.
Kidao Wilfred aliwapa shime kufanya vema kwenye mchezo wa kirafiki na
kusisitiza kambi kuendelea mpaka mchezo wa maruadiano.
Mkuu wa Msafara, Bi. Amina
Karuma, alisema kuwa mapambano bado yanaendelea na anaamini kikosi chake
kitashinda katika mechi ya marudiano itakayochezwa baada ya wiki mbili.
Karuma pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake
Tanzania (TWFA).
Aliongeza kuwa anashikuru
wachezaji wote ni wazima na wataendelea na kambi ili kujiandaa na mchezo
wa marudiano huku akiahidi kuwatafutia mechi ya kirafiki kabla ya
kuwakaribisha Nigeria.
0 comments:
Post a Comment