Na alanus
Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kuwa wakweli katika kesi ya
kutakatisha fedha na kugushi inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba,
Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange `Kaburu`.
Wakili wa serikali
Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Victoria Nongwa alidai kuwa
upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kwamba kuna nyaraka
zinamaliziwa kufanyiwa kazi.
Wakili upande wa
utetezi Philemon Mtakyamirwa alidai kuwa ni mara ya tatu upande wa
mashtaka kudai kuwa wanamalizia upelelezi hivyo aliomba tarehe ya
karibu.
Hakimu Ngongwa aliutaka upande wa mashtaka wajitahidi kuwa wakweli na kukamilisha upelelezi.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Septemba 18 mwaka huu kwaajili ya kutanjwa.
Evans Elieza Aveva na
makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi,
kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za kimarekani 300,000.
Katika shtaka la
kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu
ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba
inalipa mkopo wa Dola za kimarekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si
kweli.
Katika shtaka la pili
alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe
Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya
kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.
Katika la tatu la
kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na
Juni 29,2016 Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha
fedha kwa kupata Dola za kimarekani 300,000 wakati wakijua ni zao la
uhalifu.
Kwa upande wa shtaka
la nne la kutakatisha fedha,Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016
katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola za kimarekani 300,000
wakati akijua zimetokana na kughushi.
Katika shtaka la tano
la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa Machi 15,2016
katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidiaAveva kujipatia
Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na
kughushi.
Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.
0 comments:
Post a Comment