Tuesday, October 12, 2021



 DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba imeelezwa kuwa anapata tabu kupanga kikosi cha timu hiyo kwa sasa bila ya uwepo wa viungo wake wawili, Clatous Chama na Luis Miquissone.

Habari kutoka chanzo cha kuaminika zimeliambia Championi Jumatatu kuwa licha ya uwepo wa nyota wengi wapya kwenye kikosi hicho bado Gomes anapata maumivu ikifika hatua ya kupanga kikosi cha kwanza.


“Nadhani umezitazama mechi mbili ambazo zimepita haikuwa kwenye ule ubora ambao Simba huwa wanafanya na pia kama umegundua kikosi namna ambavyo kilipangwa kilikuwa na mabadiliko makubwa.


“Kinachompa tabu Gomes kwa sasa ni namna ya kuweza kuwa na kikosi imara na kitakachoweza kucheza bila ya uwepo wa Chama na Luis, hawa wachezaji wawili walikuwa ni wachezeshaji wa timu sasa kuondoka kwao kwa wakati mmoja ni jambo ambalo hata wewe ungekuwa mwalimu lazima ungepata maumivu kupanga kikosi cha kwanza,” ilieleza taarifa hiyo.


Kuhusu wachezaji wake wapya, Didier Gomes aliliambia Championi Jumatatu kuwa anaamini katika uwezo wa wachezaji waliopo kwa kuwa wanauwezo mkubwa ikiwa ni kwenye umiliki wa mpira pamoja na kutoa pasi.

"Wapo wachezaji wengi wapya kwa sasa ndani ya Simba na uwezo wao ni mzuri pia hivyo ni suala la kusubiri na kuona namna ambavyo watakuwa kwenye ubora,kikubwa ambacho tunahitaji ni matokoe," .

Simba ina kazi ya kusaka ushindi Oktoba 17 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

0 comments:

Post a Comment