Friday, October 15, 2021

Miaka miwili baada ya tuzo ya Ballon d'Or kutolewa kwa Lionel Messi, sherehe za tuzo hizi zinarejea tena mwaka huu kumtambua mchezaji aliyefanya vizuri zaidi mwaka huu. Tuzo hizi zinafanyika mwaka huu baada ya kuahirishwa mwaka 2020 kutokana na janga la Corona na tayari orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo hiyo ya juu kabisa mwaka huu inayotolewa kwa mchezaji binafsi imeshawekwa wazi.

Waafrika wawili Mohamed Salah kutoka Misri anayechezea klabu ya Liverpool na Riyad Mahrez kutoka Algeria anayechezea Manchester City ni miongoni mwa wachezaji 30 wanaowania tuzo hiyo.

Tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo mwaka 1956, ni mwafrika mmoja tu George Weah ambaye sasa ni rais wa Liberia, aliyewahi kutwaa tuzo hiyo, mwaka 1995. Lakini wapo wachezaji kadhaa wa Afrika waliokaribia kabisa kuibeba tuzo hiyo, lakini pengine uwepo wa Lionel Messi (Argentina) anayekipigia PSG aliyetwaa mara 6 na Cristiano Ronaldo (Ureno) wa Manchester United aliyetwaa mara 5 umepunguza fursa kwa waafrika wengi.

Nyota hawa wawili katika kipindi cha muongo mmoja uliopita wamekuwa watawala wa soka, wakibadilishana hii tuzo wao wawili. Katika miaka 14 iliyopita tangu 2008 ni mwaka 2019 pekee alitwaa Luka Modric wa Croatia na klabu ya Real Madrid, huku mwaka jana haikufanyika, lakini miaka mingine yote wamekuwa wakibadilishana.

Roger Milla, Abedi Pele, Nwanko Kanu, Jay-Jay Okocha, El Hadji Diouf na Yaya Toure haya ni majina makubwa kabisa katika soka la Afrika hakuna shaka kuhusu uwezo wao, lakini katika miongo miwili iliyopita, wafuatao ni wachezaji watano kutoka Afrika ambao walikaribia kabisa kutwaa tuzo hii ya Ballon d'Or.

5 Didier Drogba (Ivory Coast)

Didier Drogba ni mchezaji mkubwa Afrika, ana tuzo 4 za mchezaji bora wa Ivory coast na tuzo 2 za mchezaji bora wa Afrika. Mwaka 2006 ulikuwa mwaka mzuri kwa Drogba akitwaa ligi kuu mara mbili mfululizo akiwa na Chelsea akitoa mchango mkubwa kwa timu hiyo. Drogba aliingia 10 bora ya tuzo ya Ballon d'Or na mwaka uliofuata aliingia tano bora licha ya kushindwa kuitwaa tuzo hiyo.

Mwaka 2007, alimaliza nafasi ya nne kwenye Ballon d'Or nyuma ya Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na mshindi wa tuzo hiyo, Kaka. Mwaka huo alikaribia kutwaa tuzo ya dunia lakini alishindwa hata kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika, tuzo iliyokwenda kwa Frederic Kanoute, kutoka Mali.

4: Riyad Mahrez (Algeria)

Mahrez ni moja wa vipaji vikali kwenye historia ya soka Algeria, akiiongoza timu yake ya taifa kutwaa kombe la AFCON mwaka 2019.

Nahodha huyo wa Algeria ana kipaji kikubwa cha soka, akionekana kama dhahabu kuwahi kutokea kwenye soka la nchi hiyo. Mbali na kuwika na kutwa amataji akiwa na Manchester City, lakini soka lake la mwaka 2016 liliisaidia kuipa Leicester City taji la kihistoria la Ligi kuu England. Msimu huo alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa ligi hiyo

Kwa mafanikio hayo, Mahrez aliingia 10 bora ya tuzo ya Ballon d'Or na kumaliza nafasi ya 7 ambayo wengi walimtabiria angeingia 5 bora. Hata hivyo kwa nafasi hiyo, ni mafanikio makubwa kwake.

3: Sadio Mane (Senegal)

Sadio Mane ni miongoni mwa magwiji wa soka Afrika na Senegal. Katika tuzo za Ballon d'Or Mane alimaliza nafasi ya 23 mwaka 2017, nafasi ya 22 mwaka 2018 lakini mwaka 2019 ulikuwa mwaka mzuri aliokaribia kutwaa tuzo hiyo akishika nafasi ya 4. Kama isingekuwa kulikosa kombe la AFCON Senegal ilipofungwa na Algeria kwenye fainali huenda angekuwa mwafrika wa kwanza tangu George Weah kutwaa tuzo huyo ya Ballon d'Or.

Hata hivyo Mane ana muda wa kutwaa tuzo hiyo kama atafanya vyema akiwa na Klabu yake ya Liverpool na timu yake ya Senegal kwenye mashindano mbalimbali yajayo. Anahitaji tu kura za kutosha

2: Mohamed Salah (Egypt)

Kwa sasa Salah anaonekana kama mchezaji bora duniani, kiwango chake katika misimu mitatu iliyopita akiwa na Liverpool, kinadhihirisha ubora wake na namna anavyoweza kuingizwa kwenye orodha ya magwiji wa soka kutoka Afrika.

Aliiongoza Misri katika kombe la dunia 2018 na amefanikiwa kumaliza kwenye sita bora ya tuzo ya Ballon d'Or mara mbili mfululizo kuanzia mwaka 2018. Mwaka 2018 alishika nafasi ya 5, na mwaka 2019 akawa wanne nyumba.

Ana nafasi nyingine msimu mwaka 2022 kutwaa tuzo hiyo ya Ballon d'Or kama ataendelea na kiwango chake cha sasa akiwa na Liverpool pamoja na Misri, ambayo inatarajiwa kuwemo kwneye mataifa matano yatakayofuzu kombe la dunia mwakani.

1: Samuel Eto'o (Cameroon)

Inawezekana huyu ndiye mchezaji bora wa Afrika kuwahi kutokea, licha ya majina mengine mengi kuwepo kama Roger Milla, Abedi Pele, Nwanko Kanu, Jay-Jay Okocha, El Hadji Diouf na Yaya Toure. Eto'o ameshinda makombe mawili ya AFCON akiwa na Cameroon. Ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mara nne, na anatajwa ndiye muafrika aliyekaribia zaidi kutwaa Ballon d'Or.

Katika maisha yake ya soka, ameorodheshwa kwenye tuzo ya Ballon d'Or mara 10, ikiwa ni mara nyingi zaidi kuliko muafrika mwingine yoyote. Kwa mara ya kwanza Eto'o kuingia kwneye orodha hiyo ilikuwa mwaka 2004 alipomaliza wa 15, na katika miaka 8 iliyofuata hakuwa anakosa kwenye orodha ya juu ya wanaowania tuzo hio.

Alimaliza nafasi ya 10 kwenye Ballon d'Or ya mwaka 2005, mwaka 2006 alimaliza wa 7, 2007 akawa wa 30, 2008 wa 17, kabla ya mwaka 2009 akiwa na kiwango kikubwa kabisa kuingia 5 bora. Kufunga na kiwango bora kila mwaka akiwa na nyota kama Ronaldinho, Deco na Messi aliyekuwa anachipukia, E'too wa Barcelona na baadae Inter Milan iliyotwaa ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 2010 alikuwa moto wa kuotea mbali. Wengi walimuona kama alistahili kutwaa tuzo hiyo katika wakati wake.



0 comments:

Post a Comment