Friday, December 31, 2021

 



KIPA wa Polisi Tanzania, Metacha Mnata amesema tangu aanze kukaa golini hajawahi kukutana na changamoto kama aliyowahi kupata kutoka kwa aliyekuwa kiungo wa Simba, Clatous Chama.

Metacha alisema Chama alikuwa hatabiriki akiwa na mpira kama anaweza akatoa pasi, ama kuwachenga mabeki na wakati mwingine kupiga moja kwa moja.

Alimwelezea Chama ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni waliowahi kuleta chachu ya ushindani Ligi Kuu Bara, kutokana na kutumia akili zaidi kuwajibika na kuipa timu yake matokeo mazuri.

Alisema kuna wakati mwingine alikuwa anakereka kwa tabia yake ya kuwahadaa mabeki kwenda mbele bila mpira, huku akisalia nao nyuma kisha kutoa asisti ya bao.


“Kwa wachezaji wa mbele waliowahi kunipa changamoto uwanjani ni Chama, jamaa ni hatari. Unapofikiria anapiga shuti, unashangaa katoa pasi kwa mwingine kafunga,” alisema Metacha na akaongeza;

“Kuna jambo la kujifunza kwa wachezaji wa nafasi yake namna anavyotumia akili kubwa kuinufaisha Simba. Ndiyo maana hakuwa na matukio mengi ya kuadhibiwa uwanjani.”

Alitolea mfano alivyoukubali ubora wa kipa wa Yanga, Djigui Diarra kwani ameona ni somo zuri kwa makipa wazawa, nafasi anayocheza na kusisitiza kujifunza siyo dhambi, bali ni kuongeza maarifa ya kazi.


“Kusema ukweli kuna wachezaji wa kigeni ambao wameleta chachu ya ushindani mbele ya wazawa na siyo dhambi kujifunza kutoka kwao,” alisema.

Ukiachana na kumzungumzia Chama, alimtaja Kelvin Yondani kama beki mahiri anayejua kuiongoza timu na kukemea pindi baadhi ya wachezaji wanapofanya uzembe.

“Mabeki niliowahi kufanya nao kazi waliokuwa kwenye kiwango cha juu ni Yondani. Alijua kupanga timu na kuwasiliana na kipa ili kutokugongana kwenye majukumu, jamaa anajua na wanaocheza nafasi yake wakajifunze kitu,” alisema.

Mchezaji mwingine aliyewahi kukiri uwezo wa Chama ni mkubwa ni Farid Mussa wa Yanga ambaye alisema anachofanya hakiendani na mwili wake.


“Kama si umakini unaweza ukadanganyika na mwili wa Chama, lakini jamaa anajua kucheza na anatumia akili kubwa,” alisema Farid alipofanya mahojiano na gazeti hili.

0 comments:

Post a Comment